Tuesday, April 6, 2010

Waajiri wawatisha wafanyakazi

Sadick Mtulya

WAKATI Rais Jakaya Kikwete alitumia muda mwingi wa hotuba yake ya kila mwezi kusihi wafanyakazi wakubali kuingia kwenye mazungumzo badala ya kugoma, Chama cha Waajiri Tanzania(ATE) kimeamua kutoa tishio kwa wote ambao watashiriki kwenye mgomo uliopangwa kufanyika kuanzia Mei 5.

Mgomo huo umeitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) kwa lengo la kuishinikiza serikali kusikiliza madai yao baada ya kuyapuuza kwa muda mrefu na tayari shirikisho hilo lilishafuata taratibu kwa kutoa notisi ya siku 60 ambazo ziliisha bila ya serikali kuchukua hatua.

Miongoni mwa madai hayo ni kutangazwa kwa kima cha chini cha mishahara, vyombo vilivyoundwa kushughulikia masuala ya wafanyakazi kutofanya kazi na kupanua wigo wa kodi ili kumpunguzia mfanyakazi mzigo, na Rais Kikwete alikiri kuwa mishahara ni midogo na akaahidi kuipandisha.

Lakini ATE ilisema jana kuwa mgomo huo si halali na kuagiza waajiri watakaoathirika na mgomo huo wa nchi nzima, kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi watakaoshiriki, ikiwa ni pamoja na kuwaachisha kazi, kutowalipa mishahara kwa kipindi cha mgomo na hata kuajiri wafanyakazi mbadala.

ATE pia imesema iwapo mgomo huo utatekelezwa, waajiri watakaoathirika watakuwa na haki ya kudai fidia kwa hasara itakayosababishwa na mgomo pamoja na kwenda Mahakama ya Kazi kuomba nafuu za kisheria.

Mkurugenzi mtendaji wa ATE, Dk Aggrey Mlinuka alisema sheria zilizopo hazilindi wafanyakazi wa sekta binafsi wanaoshiriki migomo haramu na kwamba sekta binafsi ina taratibu zake za kuhakikisha na kulinda maslahi ya wafanyakazi.

“Pia, mgomo huu ni haramu kutokana na kwamba kifungu cha sheria namba 85 kilichotumiwa na Tucta hakihusu mgomo usiokuwa na mwisho ila kinahusu protection action (kitendo cha kulinda),” alisema Dk Mlinuka.

“Waajiri watakaoathirika na mgomo huo wawachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi watakaoshiriki mgomo huo ikiwemo kuwaachisha kazi, kutowalipa mishahara kwa kipindi cha mgomo na hata kuajiri wafanyakazi mbadala.”

Awali, mwenyekiti wa ATE, Wakili Cornelius Kariwa alisema wamefika hatua ya kupinga mgomo huo baada ya kuchunguza kwa makini sababu saba zilizotolewa katika notisi iliyotolewa na Tucta kuwa hazijitoshelezi kutangaza mgomo huo.

“Tucta haijaweka bayana Tume ya Mishahara ya Ntukamazina ilipendekeza nini. Tujuavyo sisi ripoti husika ilikuwa ni ya siri na ilikuwa kwa matumizi ya rais aliyeiteua. Isitoshe Tucta inaelekea kumlazimisha rais atekeleze mapendekezo ya Tume yasiyoainishwa.

Tunaamini huku ni kwenda kinyume na katiba ya nchi kwa kuingilia madaraka ya rais,” alisema Kariwa.

Tucta pia inaitaka serikali kuongeza wigo wa walipa kodi ili kuwapunguzia mzigo wafanyakazi ambao ni rahisi kuwafuatilia, lakini Kariwa alisema idadi ya wafanyakazi katika sekta rasmi ni ndogo na hivyo hawawezi kulipa kodi za kutosheleza mahitaji ya kuendesha nchi.

Kuhusu Wizara ya Kazi kutotangaza maamuzi yake kuhusu mapendekezo ya utafiti unaohusu kima cha chini katika sekta binafsi, Kariwa alisema hakuna sheria inayounda taasisi ya kutafiti kima cha chini vya mishahara.

“Taasisi zilizopo ni bodi za kisekta za mishahara ambazo zina jukumu la kushauri juu ya kima cha chini cha mishahara. Dai la Tucta hapa ni kuhusu kutangazwa kwa mapendekezo ya mshauri mwelekezi ambaye ni Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Economic Research Bureau).

“Tunachojua ni kwamba taarifa ya utafiti wa Mshauri Mwelekezi pamoja na maoni ya bodi za kisekta za mishahara yalijadiliwa katika kikao cha mwisho cha Baraza la Ushauri la Uchumi na Jamii (LESCO) lililokutana Machi 25, 2010. Tucta iliwakilishwa katika kikao hiki,” alisema Kariwa.

Kuhusu Wizara ya Kazi kushindwa kuunda bodi mpya za mishahara za sekta binafsi tangu zile za zamani zilipomaliza muda wake Aprili mosi, 2009, alisema bodi za mishahara za kisekta kama vilivyo vyombo vingine vya utatu vinavyoteuliwa chini ya sheria ya Taasisi za Kazi, (Na. 7 ya 2004) vilipewa uhai wa miaka mitatu toka kuundwa kwao.

“Bodi za mishahara za kisekta ziliundwa Aprili 2007 na hivyo ukomo wake utaishia mwezi huu na si kweli kwamba uhai ulikoma Aprili 2009 kama Tucta inavyodai. Tucta inatambua kwamba mchakato wa kuundwa upya kwa bodi hizi umeanza tangu Machi, 2010 na hivyo hii haiwezekani kuwa hoja ya kusababisha mgomo,” alisema Kariwa.

Kuhusu Wizara ya Kazi kushindwa kuitisha vikao vya Lesco ambacho ni chombo cha kuishauri serikali kuhusu masuala ya wafanyakazi tangu chombo hicho kizinduliwe mwezi Agosti 2009, Kariwa alisema pamoja na sheria kutofafanua lakini chombo hicho kinapaswa kukutana mara tatu kwa mwaka.

“Lwsco ilizinduliwa Agosti 2009, inabidi ifikapo Agosti mwaka huu iwe imekutana angalau mara tatu. Mpaka sasa imeshakutana mara mbili na bado tuna miezi minne kufikia Agosti,alisema.

Akizungumzia kuhusu serikali kutokuwa makini katika kurekebisha malipo dhaifu yatokanayo na Mifuko ya Pensheni ya wastaafu hivyo kuwafanya wastaafu wengi kupata mafao duni ya uzeeni, alisema mchakato wa kurekebisha matatizo yaliyopo katika mifuko hiyo ulishaanza.

Hata hivyo, ATE imeiomba Tucta kushiriki kwa dhati katika majadiliano yenye lengo la kutafuta muafaka.

“Kwa hili hakuna njia ya mkato. Tucta itambue kwamba majadiliano baina ya wadau yanajenga hali ya kuaminiana na mahusiano mazuri na endelevu,” alisema.

No comments:

Post a Comment