Tuesday, April 6, 2010

Mrema adai kuna siasa mgomo wa wafanyakazi

MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema, ambaye amekuwa akitoa kauli zinazoonekana kuitetea serikali ya awamu ya nne, amegeukia mgomo ulioitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), akisema una harufu ya kisiasa.

Mrema, ambaye safari hii atagombea ubunge wa jimbo la Vunjo baada ya kushindwa mara tatu katika kinyang'anyiro cha urais, alisema hayo jana jijini Dar es salaam alipokuwa akitoa salamu za siku kuu ya Pasaka za chama hicho.

Mrema, ambaye amekuwa akimsifu Rais Jakaya Kikwete katika miezi ya karibuni, aliitaka Tucta kuheshimu kauli ya rais aliyoitoa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Machi mwaka huu, akiwasihi viongozi wa shirikisho hilo kukubali kukaa mezani ili kutafuta suluhu ya matatizo ya wafanyakazi kwa njia ya mazungumzo.

“Utafiti wetu sisi TLP tumegundua kuwa mgomo wa Tucta unatokana na kushinikizwa... una mkono wa kisiasa ndani yake,” alisema Mrema.

Mrema alisema wamegundua kuwa baadhi ya viongozi wanaoshabikia mgomo huo wanatarajia kugombea ubunge katika majimbo yaliyo mikoa ya Kagera na Mara.

“Nasema hivyo kwa sababu kuna taarifa kuwa mgomo huo una msukumo wa viongozi hao kwa masilahi yao binafsi na vyama vyao hivyo ni vyema Tucta ikaheshimu kauli ya Rais ili kuweza kuepuka kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na viongozi hao kwa kuwahadaa wananchi kuwa wao wana uchungu na wafanyakazi,” alisema.

Alisema Tucta inapaswa kuheshimu kauli hiyo kwa sababu rais alionyesha unyenyekevu mkubwa kwa kuwa alitambua madhara yanayoweza kusababishwa na mgomo.

Mgomo huo, ambao umepangwa kuanza Mei 5, tayari umeshaungwa mkono na vyama mbalimbali vya wafanyakazi, hali inayoashiria kuwa nchi inaweza kusimama iwapo nia hiyo ya kugoma itatekelezwa na Rais Kikwete alizungumzia hilo akisema kuwa maslahi yake kiuchumi yatakuwa makubwa.

“Unyenyekevu aliouonyesha rais wetu ni fundisho hasa kwetu viongozi na unapaswa kuigwa, hivyo mkono wa maridhiano alioutoa unapaswa kupokewa na wafanyakazi wote wenye nia njema,” alisema.

Mrema alisema kutokana na ukakamavu aliouonyesha Rais Kikwete, ni muhimu vyama vya wafanyakazi vikubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo bila kumpa rais masharti yoyote.

Katika hatua nyingine Mrema aliwapongeza viongozi wa dini nchini kwa kutoa ujumbe kwa waumini wao unaosisitiza amani, utulivu lakini pia kuwaonya wale wanaohubiri chuki dhidi ya serikali iliyo madarakani.

Mrema alisema viongozi hao wanaohubiri chuki wanapaswa kukumbuka kuwa amani ikitoweka hawatakuwa tena na kondoo wa kuchunga.

No comments:

Post a Comment