Sunday, April 11, 2010

Raundi ya pili Liyumba kidedea

Happiness Katabazi



MEI, 31 mwaka jana niliandika makala katika gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: “Raundi ya kwanza Liyumba kidedea.” Paragrafu ya kwanza ilikuwa na maneno yasemayo, ‘Vita dhidi ya ufisadi vilianza kwa kishindo. Kwa kishindo hichohicho itamalizika bila ya wananchi kujua imemalizika kwa namna gani.”

Nilifikia uamuzi wa kuandika makala hiyo baada ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, Mei 27 kuifuta kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, na meneja mradi majengo ya minara pacha katika benki hiyo, Deogratius Kweka.

Hakimu huyo aliifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Kiongozi Justus Mulokozi kukiri mbele ya mahakama hiyo kuwa hati ya mashtaka ilikuwa imekosewa lakini muda mfupi baada ya washtakiwa kuachiliwa walikamatwa tena.

Mei 28 mwaka jana, Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Majura Magafu, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kufunguliwa kesi mpya ya jinai Na.105/2009 ambapo mashitaka yalikuwa ni yale yale ya matumuzi mabaya na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, huku Kweka akiachwa huru.

Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba ameendelea kusota rumande kwa sababu ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka atoe fedha taslimu au kuwasilisha hati ya mali yenye thamini ya sh bilioni 110.

Aidha, Septemba 20 mwaka jana, katika gazeti hili niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, “Watanzania wategemee nini kwenye ‘PH’ ya Liyumba?”

Ndani ya makala hiyo nilimweleza DPP kwamba kama mkoba wake katika kesi hiyo haukuwa na ushahidi madhubuti ni vizuri angeiondoa mapema mahakamani ili wasipoteze muda wa mahakama na fedha za walipa kodi.

Baada kuandika makala hizo baadhi ya wanasheria wa serikali waandamizi walinipongeza kwa makala hizo kwani zina ukweli mtupu na wakaniuma sikio na kunieleza mwisho wa siku serikali itashindwa kufurukuta katika kesi hiyo na walidiriki kuifananisha kesi hiyo na ‘sinema’.

Nimewahi kuandika kuwa Sheria ya Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2006 ilitungwa kwa shinikizo la wafadhili, serikali iliburuzwa miguu kwa miaka kadhaa lakini hatimaye ilisalimu amri pale wafadhili walipotishia kuwa wasingetoa mikopo, misaada katika nchi ambazo zisingeonyesha nia ya kupambana na rushwa (ufisadi sasa), dawa za kulevya na ugaidi.

Tanzania ilisalimu amri haraka na ikatunga sheria ya ugaidi ambayo ni kinyume kabisa na haki za binadamu na ikatunga sheria ya rushwa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 ambayo inatumika hivi sasa. Kwa hiyo tunaona serikali yetu haikuwa na nia ya dhati ya kupambana na majanga hayo, ila sheria hizo zilitungwa kishabiki, kishikaji na kisanii.

Nimelazimika kutumia kumbukumbu hizo sahihi hapo juu ili ziweze kuunga mkono mada yangu ya leo ambayo nitajadili uamuzi uliotolewa April 9 mwaka huu na Kiongozi wa Mahakimu Wakazi (Edson Mkasimongwa), Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa wa kumfutia shitaka moja kati ya mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili Liyumba.

Kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kupeleka ushahidi wa kuthibitisha shitaka la pili ambalo ni la kuisababishia serikali hasara. Aidha imemuona Liyumba ana kesi ya kujibu katika shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

“Mahakama inaamini alichokizungumza Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli, katika ushahidi wake ni ukweli mtupu na ndiyo maana alivyomaliza kutoa ushahidi wake alitoka ndani ya mahakama hii kwa amani na mawakili wa serikali hawakulalamika kwamba shahidi wao ametoa ushahidi wa uongo…kwa hiyo mahakama hii inatamka kiasi cha fedha kilichoongezeka katika ujenzi wa mradi ule kilitumika kwa utaratibu wa fedha za serikali zinavyotakiwa zitumike.

“Kwa heshima na taadhima jopo hili halikubaliani na hoja ya upande wa mashitaka iliyotaka mahakama hiyo isikubaliane na hoja ya upande wa utetezi iliyosema huwezi kuthibitisha hasara katika mradi huo hadi uwe na ripoti ya mwisho ya fedha zilizotumika kwenye mradi ule kwa sababu hata ripoti hiyo ingekuwepo isingeweza kuondoa makadirio ya gharama zilizokadiriwa na mkadiriaji wa majengo wa mradi huo.

“Mahakama inasisitiza haikubaliani na hoja hiyo ya upande wa mashitaka kwa sababu katika kesi hiyo hasara iliyodaiwa amepata mwajiri wa mshitakiwa ni lazima ithibitishwe kwa namba na ripoti…sasa katika kesi hii hasara iliyopatikana haiwezi kuwa sawa na namba ya ripoti ya Mkadiriaji wa Majengo kwani majengo ya nyongeza yamejengwa …labda ingekuwa majengo hayo mengine yanayodaiwa kujengwa nje ya mkataba wa awali na fedha hazionekana hilo lingekuwa ni jambo jingine.

“Na upande wa mashitaka wenyewe kupitia mawakili wake ukiri mbele yetu kwamba makadirio ya awali yaliyapaswa kujengwa magorofa 14 lakini baada ya mabadiliko ya ongezeko la ujenzi ziliongezeka ghorofa tatu nyingine juu hivyo kufanya kuwa na majengo mawili na kila jengo lina ghorofa 17 kwenda juu na kweli majengo yamejengwa …

“Kwa maelezo hayo mahakama hii inamfutia mshitakiwa shitaka la pili kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 an na akaueleza upande wa mashitaka upo huru kukata rufaa kama haujalidhika na uamuzi huo,” alisema Mkasimongwa na kusababisha ndugu na jamaa wa mshitakiwa wakisikika kwa sauti wakisema, ‘Asante Yesu.’

Kutokana na uamuzi huo wa Hakimu Mkazi Mkasimongwa na wanajopo wenzake, umedhihirisha pasipo shaka kwamba wachunguzi wa TAKUKURU ambao ndiyo walipeleleza kesi hii, na waendesha mashitaka walikuwa hawajui walichokuwa wanakifanya katika kuthibitisha shitaka hilo lililofutwa au walikuwa wakijua ila waliamua kumuandalia kumshitaki Liyumba.

kwa shitaka hilo makusudi mazima ili wamkomeshe kwasababu walijua hawezi kutimiza masharti na hivyo ni lazima angesota jela kwa sababu kisheria mahakama inapotoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa wa kesi yoyote ile ni lazima masharti hayo yatimizwe na si vinginevyo na endapo mshitakiwa anashindwa kutumiza anatakiwa aende rumande hadi atakapoyatimiza masharti husika.

Kama mawakili wa serikali ambao tunawashuhudia wakija pale mahakamani kwa mikogo huku wakiwa wanayaburuza masanduku kama wamehifadhi nyoka kwenye masanduku hayo na kuvalia suti utadhani ni wachungaji waliokimbiwa na waumini’ kama hawana taaluma ya kutosha kwa nini wasiombe ushirikiano wa kitaalum toka kwa mawakili wengine wenye ujuzi ambao mawakili wengine binafsi walikuwa walimu wenu vyuoni?

Serikali sasa iache uchoyo na ukiritimba katika mambo ya kitaaluma, ipende kushirika wanataluuma wenye uwezo kwenye maeno yao. Naomba kutoa hoja.

Nayasema haya kwa uchungu kwasababu ni kodi za wanachi ndizo zilizowasomesha mawakili wengi wa serikali na ndizo zinazotumika kuwalipa mishahara na fedha hizo za wavuja jasho zinazotumika kuwaweka hotelini baadhi ya mawakili wanakwenda kujichimbia katika hoteli hizo kuandika hoja mbalimbali katika kesi zilizofunguliwa na jamhuri.

Kama hawa mawakili wa serikali wanapokea mishahara inayotokana na kodi zetu, wananchi tuna haki ya kuhoji mambo wanayoyafanya ambayo hayaturidhishi.

Baadhi ya mawakili wetu wa serikali wanaonekana kuwa dhaifu na wababaishaji katika kesi wanazozisimamia na wakati mwingine nimekuwa kijiuliza akilini mwangu ubabaishaji huo unatokana ama wakati wapo vyuoni walikuwa wakiangalizia majibu kutoka kwa wenzao au walikuwa wakiiba mitihani.

Sasa kubabaikababaika kwa mawakili wa serikali waliokuwa wakiongozwa na Juma Mzarau aliyekuwa akisaidiwa na Prosper Mwangamila na Ben Lincolin katika kesi ya Liyumba hadi kusababisha mahakama hiyo awali kumfutia kesi mshitakiwa kwa sababu hati ya mashitaka ilikuwa imekosewa na juzi Hakimu Mkazi Mkasimongwa kumfutia shitaka moja mshitakiwa kwasababu upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka hilo la kusababisha hasara ni dhahiri ni ishara mbaya kwa shitaka lilobaki.

La matumizi mabaya, Watanzania sasa tujiulize kama jamhuri imeshindwa kuthibitisha shitaka la kusababisha hasara ambapo shitaka hilo linakuja baada ya mtu kutumia ofisi yake vibaya. Je upande wa mashitaka wanauakikishiaje umma kwamba mwisho wa siku wataweza kuthibitisha shitaka la matumuzi mabaya? Hilo tuliachie mahakama kwani mwisho wa siku itatoa hukumu yake kutokana shitaka hilo, ni suala la muda, tusubiri tuone.

Je, itakapotekea watuhumiwa wa kuachiwa huru si kesi zitakuwa zimekwisha kwa kishindo kile kile kama zilivyofunguliwa kwa kishindo? Tuseme nini sasa.usanii mtupu au ufisadi mtupu unaofanywa na mawakili wetu wa serikali?

Kushindwa kufurukuta kwa serikali katika shitaka hilo, nawaomba wananchi wenzangu wawe pamoja na sisi waandishi wa habari za mahakama kufuatilia kesi kama hizi zilizosalia mahakamani mfano kesi ya matumuzi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba,Gray Mgonja na Daniel Yona; kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Mkurugenzi Fedha na Utawala wa ubalozi huo Grace Martin ili hatimaye tukoleze kiu ya Watanzania katika harakati za kupambana na ufisadi.

Mwisho kabisa naupongeza Mhimili wa Mahakama nchini kwa kujipambanua kama chombo cha kutoa haki bila upendeleo, kushinikizwa na bila kuogopa. Jopo la mahakimu wakazi linalosikiliza kesi hiyo, Mkasimongwa, Mlacha na Mwingwa kutokana na uamuzi wake juzi nadiriki kusema kuwa limefanya kazi ya kishujaa na iliyoendelea kuuletea heshima mhimili wa mahakama wa nchi yetu.

Sisi tuliokuwa tunahudhuria kesi hii tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo Januari 26 mwaka jana hadi juzi, tumeshuhudia vituko, shinikizo, ubabe uliojidhihirisha kwa wingi wa makachero waliokuwa wanaipamba mahakama ya Kisutu kwa staili tofauti kila kukicha.

No comments:

Post a Comment