Tuesday, April 6, 2010

Taasisi zilizokopesha walimu kinyemela zabanwa

TaboraTAASISI za fedha mkoani hapa ambazo ziliingia mikataba ya mikopo na wafanyakazi bila kumshirikisha mwajiri zimetakiwa kusitisha mara moja makato vinginevyo zitachukuliwa hatua za kisheria.

Baraza la Wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui lililokutana juzi mjini hapa, limeziagiza taasisi hizo kusimamisha mara moja makato hayo baada ya kitendo chao cha kukaidi kuitika wito wa mwajiri wa watumishi 166 wa halmashauri hiyo aliyeagiza kukutana na wahusika wake wanaoonekana kutojali.

Kwa kauli moja wajumbe wa kikao hicho walisema lengo la kusitisha makato hayo ni kuzilazimisha taasisi hizo za fedha kuwasilisha mikataba yao kwa mwajiri, ili kuhakiki kama ilifungwa kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

Taasisi ambazo zinahusika na hoja hiyo ni Faidika, Bayport, Blue Financial Service, Tunakopesha na Istant Credit ambazo ziliandikiwa barua Agosti 11 mwaka jana lakini hazijajibu hali ambayo inadhihirisha wazi kwamba mikataba hiyo haikufuata taratibu za kisheria.

Imefahamika watumishi hao 166 ambao ni walimu waliingia mikataba ya mikopo na taasisi hizo pasipo hata kumshirikisha mwajiri, hali ambayo inawaletea shida ya kipato kwani utakuta wengi wao wamekuwa wakiambulia chini ya robo ya mshahara.

Katika hatua nyingine, viongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Walimu Wilaya ya Uyui, wameaswa kutekeleza majukumu yao kwa uwazi ikiwemo kufuata kanuni, taratibu na sheria za vyama vya ushirika zinazowaongoza.

na Murugwa Thomas,

No comments:

Post a Comment