Thursday, April 8, 2010

TAMKO LA CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE) KUHUSU NOTISI YA MGOMO WA WAFANYAKAZI WOTE ILIYOTOLEWA NA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA TUCTA

Chama cha Waajiri Tanzania kimepokea kwa mshangao mkubwa notisi ya mgomo usio na ukomo unaohusu wafanyakazi wote wa sekta za umma na binafsi.

Sisi tunashangaa kwa sababu tunaamini katika majadiliano baina ya vyama vya wafanyakazi na waajiri ikiwemo serikali kama njia bora ya kuendeleza tija sehemu za kazi na hali bora za wafanyakazi. Ni katika majadiliano tofauti za kimsingi hupatiwa suluhu. Ni pale tu ama mazingira ya majadiliano hayapo au majadiliano yenyewe yamekwama ndipo hapo silaha ya mwisho ya wafanyakazi ambayo ni mgomo hutumika.

Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kimechunguza kwa makini sababu saba (7) zilizotolewa katika notisi iliyotolewa na Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na tumeridhika mazingira ya kutangaza mgomo hayapo kwa sasa.

Sababu saba zilizotolewa na TUCTA ni:-

1. Kutotekeleza mapendekezo ya Tume ya Mishahara ya NTUKAMAZINA ambayo iliteuliwa na Mheshimiwa Rais kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

TUCTA haijaweka bayana Tume ya Mishahara ya NTUKAMAZINA ilipendekeza nini. Tujuavyo sisi ripoti husika ilikuwa ni ya siri na ilikuwa kwa matumizi ya Mhe. Rais aliyeiteua. Isitoshe TUCTA inaelekea inataka kumlazimisha Rais atekeleze mapendekezo ya Tume yasiyoainishwa. Tunaamini huku ni kwenda kinyume na Katiba ya Nchi kwa kuingilia madaraka ya Rais.

2. Kutoliangalia suala zima la ukusanyaji wa kodi, hivyo kuwafanya wafanyakazi kuwa eneo kubwa pekee la kulipa kodi za juu wakati wafanyabiashara wakilipa kodi ndogo na wakati mwingine kukwepa.

Haiyumkiniki kudai kwamba kodi wanazolipa wafanyakazi ndizo kubwa kulinganisha na maeneo mengine. Idadi ya wafanyakazi katika sekta rasmi ni ndogo na hivyo hawawezi kulipa kodi za kutosheleza mahitaji ya kuendesha nchi. Tunakiri kunaweza kuwepo matatizo katika ukusanyaji wa kodi, lakini hatudhani suluhu ya matatizo haya ni mgomo.

3. Wizara ya Kazi kutotangaza maamuzi yake kuhusu mapendekezo ya utafiti uhusuo Vima vya chini katika sekta binafsi, kinyume na sheria inavyoagiza.

Hakuna sheria inayounda Taasisi ya kutafiti vima vya chini vya mishahara. Taasisi zilizopo ni Bodi za kisekta za mishahara ambazo zina jukumu la kushauri juu ya vima vya chini vya mishahara. Dai la TUCTA hapa ni kuhusu kutangazwa kwa mapendekezo ya Mshauri Mwelekezi ambaye ni Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Economic Research Bureau). Tunachojua ni kwamba taarifa ya utafiti wa Mshauri Mwelekezi pamoja na maoni ya Bodi za Kisekta za mishahara yalijadiliwa katika kikao cha mwisho cha Baraza la Ushauri la Uchumi na Jamii (LESCO) lililokutana tarehe 25 Machi 2010. TUCTA iliwakilishwa katika kikao hiki.

Hivo suala hili limo katika mchakato na hivyo haliwezi kuwa hoja halali ya mgomo. Hata hivyo tunajua Tangazo la Serikali Namba 223 la mwaka 2007 kuhusu vima vya chini vya mishahara bado lina nguvu za kisheria mpaka hapo Mhe. Waziri wa Kazi atakapotangaza vima vipya vya mishahara.

4. Wizara ya Kazi kushindwa kuunda bodi mpya za mishahara za sekta binafsi tangu zile za zamani zilipomaliza muda wake 1 Aprili 2009.

Tunavyofahamu sisi, Bodi za mishahara za kisekta kama vilivyo vyombo vingine vya utatu vinavyoteuliwa chini ya sheria ya Taasisi za Kazi, (Na. 7 ya 2004) vilipewa uhai wa miaka mitatu toka kuundwa kwao. Bodi za mishahara za kisekta ziliundwa Aprili 2007 na hivyo ukomo wake utaishia mwezi huu na si kweli kwamba uhai ulikoma Aprili 2009 kama TUCTA inavyodai. TUCTA inatambua kwamba mchakato wa kuundwa upya kwa Bodi hizi umeanza tangu Machi 2010 na hivyo hii haiwekani kuwa hoja ya kusababisha mgomo.

5. Wizara ya Kazi kushindwa kuitisha vikao vya LESCO ambacho ni chombo cha kuishauri serikali kuhusu masuala ya wafanyakazi tangu chombo hicho kizinduliwe mwezi Agosti 2009 licha ya Raisi kuagiza likutane katika kikao chetu cha 4/5/2009 Ikulu Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa sheria, LESCO inapaswa kukutana angalau mara tatu (3) kwa mwaka. Sheria haijafafanua ni kipindi gani katika mwaka. LESCO iliyopo ilizinduliwa Agosti 2009, inabidi ifikapo Agosti mwaka huu iwe imekutana angalau mara tatu. Mpaka sasa imeshakutana mara mbili na bado tuna miezi minne kufikia Agosti. Hivyo hatuoni utoshelevu wa sababu hii kuhalalisha mgomo.

6. Ofisi ya Waziri anayehusika na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kushindwa kuitisha vikao vya majadiliano yanayohusu maslahi ya watumishi wa umma kama sheria ya majadiliano (The Public Service Negotiating Machinery) Act 2003 inavyoagiza.

Hatuoni sababu hii kutosheleza kuita mgomo wa nchi nzima kwa kujumuisha hata wafanyakazi wa sekta binafsi ambao wana utaratibu tofauti wa majadiliano.

7. Serikali kutokuwa makini katika kurekebisha malipo dhaifu yatokanayo na Mifuko ya Pensheni ya Wastaafu hivyo kuwafanya Wastaafu wengi kupata mafao duni ya uzeeni.

Mchakato wa kurekebisha matatizo yaliyopo katika mifuko ya hifadhi ya jamii ulishaanza. Wadau wote katika utatu ikiwemo TUCTA tunafahamu mchakato unaoendelea wa kuunda Mamlaka ya kusimamia mifuko hii (Social Security Regulatory Authority). Kwa kuwa hili ni suala la kimchakato na linalohitaji uangalifu mkubwa, ni maoni yetu kuwa TUCTA imekosa subira inayohitajika kwa jambo muhimu kama hili. Si haki hata kidogo kumlaumu binafsi. Mhe. Waziri wa Kazi. Kwa maana hii hatuoni sababu yeyote ya msingi ya kuitisha mgomo kwa hoja hii.

HITIMISHO

Kutokana na ufafanuzi huu, Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) kinatamka kama ifuatavyo:-

1. Kwamba Notisi iliyotolewa ni wa mgomo usio halali kwa kuwa:-
a) Sababu za mgomo hazipo
b) Njia za majadiliano bado zipo wazi na wala majadiliano hayajashindikana
c) Mgomo uliotangazwa hauna kipindi maalum kinyume na matakwa ya kisheria
d) Mgomo uliotangazwa unahusu sekta zote za uchumi wa nchi ikiwemo sekta binafsi ambayo ina taratibu zake za kuhakikisha na kulinda maslahi ya wafanyakazi.
e) Mgomo huu utahusu pia sekta ya huduma muhimu kwa jamii (essential services) ambazo haziruhusiwi kisheria kugoma.

2. Kwa kuwa mgomo huu si halali, Waajiri watakaoathirika watakuwa na haki ya kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi watakaoshiriki mgomo huu haramu ikiwemo kuwaachisha kazi; kutowalipa mishahara kwa kipindi cha mgomo na hata kuajiri wafanyakazi mbadala. Ijulikane kwa wadau wote kwamba sheria zilizopo hazilindi wafanyakazi wanaoshiriki migomo haramu.

3. Iwapo mgomo huu utatekelezwa, Waajiri watakaoathirika watakuwa na haki ya kudai fidia kwa hasara itakayosababishwa na mgomo dhidi ya TUCTA ilioitisha mgomo usio halali.

4. Waajiri wanayo haki ya kwenda Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi (Labour Division) kuomba nafuu za kisheria.

Tunatoa RAI kwa TUCTA na wadau wote waliohamasishwa na TUCTA, waachane na harakati za kuitisha mgomo ambao utakuwa ni hasara kwa pande zote. Tunainasihi TUCTA washiriki kwa dhati majadiliano yenye lengo la kuleta muafaka wa pamoja. Kwa hili hakuna njia ya mkato. TUCTA itambue kwamba majadiliano baina ya wadau yanajenga hali ya kuaminiana na mahusiano mazuri na endelevu.

Ikumbukwe kwamba amani na utulivu sehemu za kazi ni nguzo muhimu za kuongeza tija, kukuza uchumi, kuwepo kwa ajira endelevu na kupambana na umaskini. Vyama vya Wafanyakazi ni wadau muhimu katika kuendeleza amani na utulivu mahali pa kazi.

Dar es Salaam, 5 Aprili 2010
CHAMA CHA WAAJIRI TANZANIA (ATE)


Wakili Cornelius K. Kariwa
Dkt. Aggrey K. Mlimuka
MWENYEKITI MKURUGENZI MTENDAJI

No comments:

Post a Comment