Friday, April 30, 2010

MATOKEO KIDATO CHA SITA: Shule za Serikali zaibuka kidedea

Boniface Meena

SHULE za sekondari za serikali zimeng'ara katika matokeo ya kidato cha sita baada ya wanafunzi wake tisa kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa.Lakini shule hizo za serikali hazikuweza kufua dafu kwa upande wa wasichana baada ya shule binafsi kutoa wanafunzi nane kati ya kumi bora waliofanya vizuri kwenye mtihani huo wa kumaliza elimu ya juu ya sekondari.

Wanafunzi wote walioshika nafasi kumi za kwanza ni wavulana. Wanafunzi hao ni Japhet John wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Manyanda Chitimbo (Kibaha, Pwani), Hassan Rajab (Minaki, Pwani), Abdulah Taher, Stinin Elias, Paul Nolasco na Ephraim Swilla wote kutoka Mzumbe, Morogoro.

Wengine ni Alexander Marwa na Benedicto Nyato kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora, wakati Samuel Killewo wa Shule ya Sekondari ya Feza Boys ndiye mwanafunzi pekee kutoka shule binafsi aliyeingia kumi bora.

Kwa upande wa shule za wasichana, Jacqueline Seni wa Shule ya Sekondari ya Marian Girls iliyo Bagamoyo mkoani Pwani ndiye aliyeongoza akiwa na wenzake Khadija Mahanga, Esther Mlingwa, Perpetua Lawi na Lilian Kakoko, wakati Gerida John na Subira Omary wanatoka Shule ya Sekondari Dakawa.

Wasichana wengine waliofanya vizuri ni Elaine Kinoti kutoka Ashira, Kilimanjaro, Ruth Pendaeli kutoka Shule ya Sekondari ya Morogoro na Cecilia Ngaiza kutoka St Joseph Ngarenaro, Arusha Cecilia.

Shule za Marian Girls, Mzumbe, Kibaha, Tabora Boys, Ilboru, Malangali, Kifungilo, Tukuyu, Feza Boys na Uru Seminary zimeingia katika kumi bora wakati shule ya High-View International, Fidel Castro, Sunni Madressa, Neema Trust, Mtwara Technical, Muheza, Tarakea, Uweleni, Arusha Mordern na Maswa Girls zimekuwa shule kumi zilizoshika mkia.

Jumla ya watahiniwa 55,764, ambao ni asilimia 88.86 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo mwaka huu, wamefaulu na kati ya hao wasichana waliofaulu ni 21,821 (sawa na asilimia 90.39) ya waliofanya mtihani na wavulana waliofaulu ni 33,943 (sawa na asilimia 87.90 ya wavulana waliofanya mtihani).

Kwa kulinganisha na mwaka jana wakati waliofaulu walikuwa wanafunzi 45,217 (sawa na asilimia 89.64), idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa wanafunzi 10,048, hata hivyo asilimia ya ufaulu imepungua kidogo kwa asilimia 0.78 mwaka huu.

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani(Necta), Dk Joyce Ndalichako alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 45,217 sawa na asilimia 93.76 ya waliofanya mtihani; wasichana waliofaulu ni 17,905 sawa na asilimia 94.07 na wavulana ni 27,320 sawa na asilimia 93.56.

“Ukilinganisha idadi hiyo na mwaka jana ambapo watahiniwa 36,472 sawa na asilimia 94.37 ya watahiniwa wa shule waliofaulu, idadi ya waliofaulu imeongezeka mwaka huu kwa wanafunzi 8,745 wakati asilimia ya ufaulu imeshuka kidogo kwa asilimia 0.61,” alisema Dk Ndalichako.

Kwa watahiniwa wa kujitegemea, Dk Ndalichako alisema waliofaulu mtihani ni 10,547 sawa na asilimia 72.57 ya wote na kwamba ikilinganishwa na mwaka jana watahiniwa 9,244 sawa na asilimia 74.84 walifaulu, hali inayoonyesha kuwa idadi ya waliofaulu imeongezeka kwa watahiniwa 1,303.

Dk Ndalichako alisema kuwa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 39,625 (sawa na asilimia 82.17) wamefaulu kati daraja la kwanza hadi la tatu, wakiwemo wasichana 15,650 (sawa na asilimia 82.22) na wavulana 23,975 (asilimia 82.13).

“Hata hivyo Necta imesitisha kutoa matokeo ya kwa watahiniwa 484 ambao hawajalipa ada ya mtihani na matokeo yao yatatolewa mara watakapolipa ada,” alisema.

Pia imesitisha matokeo ya watahiniwa 49 waliofanya mtihani huku wakiwa na sifa zenye utata matokeo yao yatatolewa mara watakapowasilisha vyeti vyao halisi vya kidato cha nne kwa ajili ya uhakiki pamoja na vielelezo vya kuthibitisha uhalali wao.

Mbali na kufuta matokeo hayo, Necta luimefuta matokeo ya mwaka 2009 kwa watahiniwa 31 wa shule na watahiniwa 105 wa kujitegemea waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo.

“Mwaka 2009 watahiniwa nane wa shule na watahiniwa 17 wa kujitegemea walibainika kufanya udanganyifu na matokeo yao yote yalifutwa,” alisema Dk Ndalichako.

Alisema kuwa watahiniwa watatu pia wamefutiwa matokeo yao baada ya kufanya mtihani bila kuwa na sifa zinazostahili ikiwa ni pamoja na kughushi vyeti au kutumia sifa za watu wengine.

Akizungumza na Mwananchi, Jackline Seni, ambaye aliongoza kwa upande wa wasichana, alisema anamshukuru Mungu kwa yote na kwamba sasa ana uhakika wa atasoma Chuo kikuu chochote kile duniani.

Seni, ambaye anaishi Kijitonyama jijini Dar es salaam, alisema kuwa haamini kilichotokea lakini anamshukuru Mungu kwa yote.

“Yani we acha tu sikutegemea hivi, lakini nimeonyesha kuwa wanawake tunaweza,” alisema Jackline ambaye alikuwa akichukua masomo ya uchumi, jiografia na hesabu (EGM).

Alisema kuwa matokeo hayo yamempa faraja kwa kuwa hata katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2007 alikuwa wa nne kitaifa na aliongoza katika somo la hesabu na fizikia.

Alisema alipenda kuwemo katika kumi bora ya jumla kwa kuwashinda wavulana, lakini alichokipata kinamtosha kwa kuwa ana uhakika wa kusoma chuo kikuu chochote hapa nchini na nje ya nchi.

“Ninachoomba ni niweze kufanya vizuri huko chuoni na kumaliza vyema kama ilivyokuwa huko nyuma... naamini wasichana na wanawake kwa ujumla tunaweza na tutafika mbali,” alisema Jackline Seni ambaye aliwakumbuka wenzake wa Shule ya Mirian Girls na kuwataka wafanye vizuri zaidi na kuitangaza shule hiyo.

No comments:

Post a Comment