Saturday, April 3, 2010

TUCTA YAMVIMBIA JK

YASEMA KUAHIDI ONGEZEKO LA MSHAHARA NI KUVUNJA SHERI

SHIRIKISHO la Vyama Vya Wafanyakazi (Tucta) limekataa wito wa Rais Jakaya Kikwete wa kutaka wamalize matatizo yao kwa njia ya mazungumzo, likisema labda mkuu huyo wa nchi aitishe kikao kitakachowahusisha watendaji wake.

Tucta imeshatangaza kuwa mgomo huo wa nchi nzima utafanyika kuanzia Mei 5 na kwamba haitamwalika rais siku ya sherehe za Mei Mosi na badala yake mwenyekiti wa shirikisho hilo ndio atakuwa mgeni rasmi na siku hiyo itatumika kuzungumzia matatizo ya wafanyakazi na mgomo.

Tucta inadai kuwa kwa muda mrefu serikali imepuuza madai ya wafanyakazi ambayo ni pamoja na ongezeko la mshahara, kupunguziwa kodi inayokatwa kwenye mishahara, malipo kidogo kwa wastaafu na wizara kushindwa kuitisha mikutano ya Lesco.

Lakini Rais Kikwete alijibu madai yao kwa kuwasihi viongozi wa Tucta kukubali kukaa mezani ili matatizo hayo yaishe kwa mazungumzo na kwamba serikali iko mbioni kupandisha mishahara licha ya ufinyu wa bajeti.

Jana naibu katibu mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema kuwa Rais Kikwete amedanganywa na mawaziri wake kuhusu chanzo cha mgomo huo na hivyo hotuba yake juzi haikujitosheleza.

"Tumepokea hotuba yake na maombi yake tumeyasikia, lakini tunasikitika kuwa mambo mengi aliyoyazungumza yanaonyesha mawaziri wake wanamdanganya, njia pekee ni kwa yeye kukutana na sisi katika mazungumzo ambayo yatahusisha mawaziri wake ili tuyawake bayana mambo hayo," alisema

Alifafanua kuwa katika hotuba hiyo, rais anaonekana alidanganywa kuwa Tucta ilikutana na Tume ya Utumishi wa Umma katika vikao vya majadiliano mara sita, wakati si kweli. Alisisitiza kuwa hawakutana katika kikao chochote na tume hiyo.

Mgaya alimshambulia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia na Waziri wa Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana, Juma Kapuya kuwa ndio wanaompotosha rais kwa kutomweleza ukweli kuhusu suala hilo.

Mgaya alifafanua kuwa katika hotuba yake ya juzi rais alizungumzia dai moja kati ya madai matatu na akaipinga ahadi ya mkuu huyo wa nchi ya kupandisha mshahara, akidai kuwa kuahidi kwa jinsi hiyo ni kinyume na sheria.

"Sheria inataka kuwapo kwa majadiliano baina ya wafanyakazi na waajiri wake juu ya suala la kupandishwa kwa mishara na madai mengine kabla ya kutekelezwa kwake majadiliano hayo ambayo huhitimishwa Desemba 15 yanalenga kutoa fursa kwa vipengele vya makubaliano kuingizwa kwenye bajeti.

"Vikao hivyo havijafanyika leo tunakwenda kujadili nini wakati bajeti ya kwa mwaka huu iko tayari," alisema Mgaya.

Kwa mujibu wa Mgaya, kitendo cha Rais Kikwete kuwaeleza kuwa atapandisha mshahara bila kuwapo makubaliano ni kinyume na sheria kwa kuwa maamuzi hayo yanahusu upande mmoja na yanaweza kutoa mwanya kwa serikali kulipa mishahara midogo kinyume na matarajio ya wafanya kazi.

Alisema kimsingi ili mshahara upandishwe, majadiliano baina ya wafanyakazi na waajiri yanatakiwa na kwamba baadhi ya vipengele vitakavyotokana na majadiliano hayo ndivyo vitakavyoingizwa kwenye bajeti kwa ajili ya kuombewa fedha.

Mgaya alisema kitendo cha rais kutoyazungumzia madai mengine ya wafanyakazi kwenye hotuba yake ni ishara nyingine kwamba hajaelezwa kila kitu kinachosababisha maandalizi ya mgomo huo yanayosimamiwa na mwenyekiti wa kamati, Gratian Mukoba.

Alitaja madai mengine kuwa ni malipo kidogo wanayoyapata wafanyakazi wanapostaafu kutoka kwenye mifuko ya kijamii na kodi kubwa wanayotozwa wafanyakazi kutoka kwenye mishahara yao.

Alisema walishatoa ushauri mara kadhaa kwa serikali kupanua wigo wa kukusanya kodi ili kupunguza mzigo kwa wafanyakazi kwa kuwa kuna kundi la Watanzania ambao hawalipi kodi, lakini serikali haijashughulikia.

Mwenyekiti wa kamati ya mgomo huo, Gratian Mkoba alisema kwa sasa wafanyakazi hao hawako tayari kurudi kwenye meza ya mazungumzo na serikali kwa kuwa mgomo huo umefuata taratibu zote.

Kuhusu hutuba ya rais iliyotolewa juzi alisema wafanyakazi hawajaridhika nayo na kusisitiza kuwa hawawezi kurudi nyuma, labda madai yao yaingizwe kwenye bajeti ya mwaka huu.

"Ingawa tunaingia kwenye kikao kujadili suala hilo kwa sasa bado inaonekana hotuba ya rais haijaturidhisha... wafanyakazi hatujaridhika nayo; kwanza imetuongezea ajenda kwenye kikao chetu. Sisi hatutakuwa tayari kubadili msimamo wetu labda tuhakikishiwe kuwa madai hayo yanaingia kwenye bajeti ya mwaka huu," alisema Mukoba.

Juzi Rais Kikwete alikiri kuwa imekuwa inamuwia vigumu kuzungumzia mgomo wa wafanyakazi wote ulioitishwa na Tucta na akaenda mbali zaidi kuwasihi viongozi wa wafanyakazi kufikiria upya uamuzi wao.

Pia mkuu huyo wa nchi ameeleza kwa msisitizo kuwa serikali haipuuzi madai ya wafanyakazi, bali "tunawajali na kuwathamini sana wafanyakazi: wawe wa serikali au wawe wa sekta binafsi" na hivyo kuwasihi viongozi wa Tucta kukubali kufanya mazungumzo na serikali na waajiri wengine ili kumaliza mgogoro huo.

Rais Kikwete alionyesha unyenyekevu akiwasihi wafanyakazi kufanya mazungumzo kwa kuwa ndio uamuzi wenye maslahi kwa taifa badala ya kutumia mgomo.

"Lazima nikiri mapema kabisa kuwa nilipata taabu kulizungumzia jambo hili hasa kwa jinsi kauli za viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanaohamasisha mgomo huo zilivyokuwa kali," alisema Kikwete katika hotuba yake.

No comments:

Post a Comment