Walimu watatu wa kike na mke mmoja wa mwalimu wa kijiji cha Sakasaka, tarafa ya Kisesa wilayani Meatu, wamevuliwa nguo na kucharazwa viboko na walinzi wa jadi sungusungu wa kijiji hicho kwa madai ya kutohudhuria mkutano uliokuwa umeitishwa na jeshi hilo.
Imedaiwa kuwa walimu hao walishindwa kwenda kwenye mkutano huo kwa sababu ni wajawazito jambo ambalo sungusungu hao walipinga na kuwalazimisha wavue nguo kuthibitisha kama kweli ni wajawazito mbele ya mkutano huo.
Tukio hilo la aina yake na udhalilishaji kijinsia, lilitokea AprilI 7, mwaka huu kati ya saa na 4:00 na 5:00 asubuhi kijijini hapo.
Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) wa wilaya ya Meatu, Baraka Owawa, aliiambia Nipashe kuwa walimu hao walikamatwa na sungusungu hao na kuanza kuwapiga, kuwavua nguo kwa madai ya kutohudhuria mkutano.
Owawa alisema walimu hao hawakuwa na jinsi yoyote ya kukabiliana na sungusungu hao bali walitii amri hiyo ya askari hao wa jadi kunusuru maisha yao.
Mara baada ya walimu hao kufanyiwa unyama huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Julius Mtuli, alitoa taarifa kwa uongozi wa juu wilayani hapa ikiwemo polisi na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu na timu maalum kuundwa kwenda kijijini hapo kufuatilia suala hilo.
Katika kufuatilia tukio hilo, juzi timu hiyo iliyojumuisha maafisa kutoka ofisi ya Mkuu wa wilaya, Afisa Elimu wa Wilaya, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSD) Mkaguzi Mkuu wa Shule za Msingi hadi kijijini hapo na polisi kukutana na uongozi wa kijiji hicho.
Katika kikao cha pamoja na uongozi wa serikali ya kijiji, ulikiri kutokea kwa tukio hilo lakini ulisita kuwataja wahusika wa tukio hilo kwa kile kinachodaiwa ni kuogopa fitina kijijini hapo.
Aidha, uongozi huo uliomba radhi kwa walimu wote kwa niaba ya sungusungu waliofanya kitendo hicho ambalo walimu wamelilaani.
Pamoja na uongozi huo kusita, polisi wametoa amri ya uongozi wa kijiji hicho akiwemo Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, Afisa Mtendaji wa kijiji, Kamanda na Katibu Mkuu wa Sungusungu kufika kituo kikuu cha polisi cha mjini Mwanhuzi Aprili 19, mwaka huu wakiwa na taarifa kamili na majina ya wahusika waliosababisha udhalilishaji huo kwa walimu.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mtuli alisema walimu katika kijiji hicho chenye shule mbili za msingi za Sakasaka `A' na `B', wamekilaani kitendo hicho na wamekatishwa tamaa na tabia hiyo na kuomba CWT iwasaidie kumwomba mwajiri wao wahamishwe kijijini hapo.
Mwalimu huyo wa Shule ya Msingi Sakasaka `B' aliongeza kuwa wananchi wa kijiji hicho wamekuwa na tabia ya kuwadhalilisha walimu na wafanyakazi wengine wanaofanyakazi eneo hilo ikiwemo kuwapiga, kuwatishia maisha, kuwanyanyasa na kutothaminiwa.
Mei, mwaka jana, mwalimu mmoja wa kiume (jina limehifadhiwa), pia alipigwa na kuvuliwa nguo zake alizovaa na kumwacha kama alivyozaliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Abiud Saideya, alipozungumza na Nipashe kwa njia simu alikiri kutokea kwa tukio na tayari ametoa maelekezo kwa maafisa wake na kuahidi kutoa maelezo zaidi kwa kuwa yuko nje ya wilaya yake kikazi.
No comments:
Post a Comment