na Stella Ibengwe, Meatu
JESHI la Polisi wilayani Meatu, mkoani Shinyanga linamshikilia Mwenyekiti ya Mtaa wa Kisesa, Ibrahimu Karango (CUF) kwa tuhuma za kuitisha mkutano wa hadhara uliosababisha walimu watatu kuchapwa viboko na sungusungu wa Kata ya Sakasaka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Abiudi Saidea, alisema mbali ya kufikishwa katika vyombo vya sheria, mwenyekiti huyo pia wilaya imelazimika kuvunja uongozi wa sungusungu katika kata hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema sungusungu wako kisheria na waliwekwa kisheria isipokuwa wamefanya makosa kujichukulia sheria mkononi na kuongeza kuwa kwa sasa hakuna viongozi wa sungusungu katika kata hiyo hadi pale wilaya inakapokaa na kuamua nani awe kiongozi kwa kufuata taratibu zilizopo.
Alisema hizo ni hatua za awali za kuchunguza ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika katika zoezi hilo la kuwatandika viboko walimu, ambapo chanzo chake kwa kina kinachunguzwa na vyombo vya usalama.
Hata hivyo Saidea aliwataka wananchi wa Wilaya ya Meatu kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wanachunguza tukio hilo ambalo limeweka wilaya katika sura ya kipekee kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa.
Mkuu huyo wa wilaya amewaasa wanafunzi wa shule hiyo kuendelea kuwatii walimu pamoja na kufuata sheria zote za shule na si kuchukulia suala la walimu wao kutandikwa viboko kama ni njia ya kuwadharau katika utendaji wao wa kazi.
Tukio la kutandikwa viboko walimu hao lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo walimu watatu wa Shule ya Kisesa walitandikwa kwa kile kinachodaiwa kuwa walichelewa kufika katika mkutano wa sungusungu ndipo mwenyekiti wa mtaa huo alipoamua kuamrisha sungusungu kuwacharaza viboko walimu.
Tukio kama hilo la walimu kuchapwa viboko lilishawahi kutokea katika Mkoa wa Kagera ambapo walimu walicharazwa fimbo na mkuu wa wilaya.
No comments:
Post a Comment