Thursday, April 1, 2010

mbunge wa Kishapu Fred Mpendazoe kukihama Chama Cha Mapinduzi








Waandishi Wetu

HATUA ya mbunge wa Kishapu Fred Mpendazoe kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama Cha Jamii (CCJ) imekipa kiwewe chama hicho tawala baada ya makada wake kutoa kauli zinazoashiria kumkebehi huku Ridhiwan Kikwete akiwatoa hofu wanachama wa chama chake.

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mohammed Mbonde, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Wenyeviti wa mikoa wa CCM, Pancras Ndejembi, mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwan na wapigakura wa Jimbo la Kishapu jana walitoa kauli zinazotofautiana kuhusu uamuzi huo wa kihistoria.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Ridhiwan Kikwete alisema kujiondoa kwa Mpendazoe kumeonyesha kuwa wananchi walikuwa na mbunge wa aina yake na kuwasihi wamwache aende zake.

Ridhiwan ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Shinyanga kuhudhuria sherehe za kusimikwa kwa makamanda wa UVCCM wa wilaya, ziara ambayo imefanyika siku moja baada ya mbunge huyo kutangaza kuihama CCM na kujiunga na CCJ.

Alisema kuondoka kwa mbunge huyo kutoka CCM na kukimbilia CCJ ni kielelezo cha aina ya viongozi ambao wamekuwa mzigo kwa chama ambao wamekuwa wakipendekezwa na kuteuliwa kuongoza.

"Mwacheni aende Mpendazoe, kuondoka kwake kusitufanye kukosa raha sisi CCM, wapo wengi waliondoka na chama bado kipo imara, muhimu kusonga mbele,� alieleza.

Alisema Mpendazoe alikuwa akifanya mambo mengi kinyume na kanuni za chama na kuwaomba wananchi kutulia na kuangalia viongozi wengine, lakini akisisitiza kuwa walio makini na siyo wale wa kuja.

Ridhiwan alisema kuondoka kwa Mpendazoe kunapaswa kuwa fundisho kwao kuchagua viongozi wenye sifa za uongozi na wenye uwezo wa kuongoza na kutamba kuwa chama kinao wanachama wengi, hivyo wanaoondoka kwa sababu zao wajue kuwa CCM itaendelea kubaki pale pale bila ya kutetereka.

“Nawaasa viongozi kutochagua viongozi kwa kuangalia sura au fedha za mtu, bali chagueni watu wenye moyo na msimamo wa kukitetea na kuimarisha chama kwa vitendo…, huo ndio msimamo wa CCM,� alisisitiza Ridhiwan.

Awali kabla ya kuongea kwa Ridhiwan, UVCCM Shinyanga, ulitoa tamko ambalo lilisomwa na Gasper Kileo la kusema kuwa vijana wa chama hawawezi kunyamaza kimya kutokana na kitendo cha mbunge huyo kujiengua CCM.

Walisema kuwa kwa muda mrefu mwenendo mzima wa mbunge huyo ulikuwa na mwelekeo wa kukinzana na maadili ya CCM, na kwamba alichokifanya ni kukipunguza mzigo kwa vile tayari alikuwa kero ndani ya chama na jimbo lake kwa ujumla.

“Hatukujua kama tuliteua mbunge asiyekuwa na uchungu na wapigakura wake kiasi cha kuwatelekeza na kuwanyima haki yao ya kuwa na mwakilishi hasa katika kipindi hiki cha bajeti, tunaamini hakuna kitakachoharibika kwani tunatambua mshikamano wa watu wa Kishapu’’ alisema kada huyo katika tamko hilo la vijana.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, yeye alimkana Mpendazoe kwamba hakuwa kiongozi ambaye alipatikana katika mchakato wa uchaguzi yeye akiwa ni mwenyekiti bali walimkuta baada ya kupitishwa na viongozi wenzake waliowatangulia.

Alisema viongozi wenzake walikosea kumteua Mpendazoe kwa vile alifahamika na kwa kufanya kwao hivyo waliwaacha wengine wenye uwezo ambao kama wangepewa nafasi ya Mpendazoe leo bado wangelikuwa wakiendelea kuwatumikia wananchi wa Kishapu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Kishapu, Boniface Butondo alipohojiwa na Mwananchi alisema kuwa kuondoka kwa Mpendazoe kumewafanya kupumua kwa vile alikuwa kero kubwa na mwenye ugomvi jambo ambalo lilimfanya kutofautiana na madiwani walio wengi wa chama chake.

Hata hivyo, katika hafla hiyo fupi ya kuwasimika makamanda wapya wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, zilizofanyika kwenye Viwanja vya NSSF mjini, jumla ya makamanda 17 walisimikwa na Ridhiwan Kikwete kwa ajili ya wilaya za Kahama, Bariadi, Bukombe Maswa, Meatu, Shinyanga mjjini, Shinyanga Vijijini na Kishapu iliyokuwa Jimbo la Mpendazoe.

Naye Mbonde jana aliripotiwa na vyombo vya habari kuwa alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kumweleza kuwa CCM Shinyanga ilitarajia hatua hiyo ya Mpendazoe siku nyingi hivyo kilichotokea ni sawa na kuvuja kwa pakacha ambako ni nafuu ya mchukuzi.

Kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba CCM/SHR/CON.2/Vol.IV/157, katibu huyo wa mkoa alisema CCM Shinyanga ilitarajia hilo kutokana na minong'ono ya muda mrefu na mabadiliko ya tabia na mwenendo wake uliojidhihirisha katika matamshi yake ndani ya Bunge na jimboni Kishapu.

"Mheshimiwa katibu nikuhakikishie kwa dhati kabisa kuwa Jimbo la Kishapu ni mali ya CCM na ngome kuu ya chama chetu. Usishtuke sana kwani kuvuja kwa pakacha ni nafuu kwa mchukuzi. Aende salama," ilinukuliwa taarifa hiyo.

Wakati katibu huyo akitoa kauli hiyo, mwanasiasa nguli nchini, Mzee Ndejembi alisema uamuzi wa Mpendazoe kuihama CCM haujakipunguzia kitu chama hicho.

Kauli hiyo ya Ndejembi inafanana na kauli iliyotolewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa.

Lakini jana Ndejembi aliongeza kuwa uamuzi wa mbunge huyo unaonyesha kuwa CCM inakubalika kila kona ya nchi akiwataka wengine ambao wako kimasilahi waondoke mapema kama alivyofanya Mpendazoe.

“Mimi nasema CCM kitaendelea kuwa ngangari na watapondwa vipande vipande katika Uchaguzi Mkuu wala watu wasitishwe na huyo Mpendazoe kwani kufanya hivyo amekiimarisha chama na kukiweka katika mazingira mazuri sana kuelekea uchaguzi � alisema Ndejembi na kuongeza:

“CCM inaongozwa kwa mujibu wa Katiba, kanuni na taratibu na hata wao walikikuta na wamekiacha na hao waliingia kwa kufuata masilahi sasa wameona malengo yao hayatimizwi kutokana na misimamo iliyopo ndani yake.�

Ndejembi alisema wapo viongozi ambao walihama CCM, lakini hadi leo chama hicho kimesimama na hakiyumbi na kuwatolea mfano kina Lipumba na Seif Sharif Hamad (CUF) ambao kuondoka kwao hakukuyumbisha chama.

Hata hivyo, alionyesha wasiwasi kuwa labda kuna jambo lililomsibu mbunge huyo mpaka akaihama CCM kwani uamuzi huo ni mzito mno kufanywa na mtu wa hadhi yake.

“Mtu mzima kulia barabarani lazima kutakuwa na jambo ama msiba au ameibiwa,� hivyo na Mpendazoe inawezekana moja kati ya hayo limemkuta.

Kiongozi mkongwe katika medani ya siasa nchini, Peter Kisumo ameeleza kuwa pamoja na jitihada za Rais Jakaya Kikwete kuweka sheria mbalimbali za kudhibiti vitendo vya rushwa bado kuna baadhi ya wabunge ndani ya chama hicho wanatoa rushwa ili wapate uongozi.

Alisema Serikali ya Awamu ya Nne imejitahidi kupingana na kadhia za rushwa hasa katika nyanja ya siasa, lakini, kutokana na sababu mbalimbali sheria hiyo itakuwa ngumu kutekelezwa hasa kwa baadhi ya viongozi waliyopo ndani ya CCM.

Mzee Kisumo alitolea mfano wa hivi karibuni wa baadhi ya wabunge kukiri kutoa vyakula na posho za nauli kwa baadhi ya wanachama wa CCM na hata kuwanunulia mavazi akieleza kuwa mambo hayo ndiyo yatakayofanya sheria hiyo ikose nguvu.

Alidai kuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro kuna kiongozi mmoja mkubwa ambaye kila wiki anafanya sherehe na kutoa zawadi mbalimbali kwa wanaofika kumuunga mkono jambo ambalo linahitaji kutolewa kwa elimu juu ya sheria hiyo mpya kabla ya kuanza kutumika.

Alisema kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kufanikisha kuwepo kwa sheria hiyo kunamfanya aonekane kuwa ni miongoni mwa viongozi wenye kujiamini na kutoa mfano kwa viongozi wengine ndani na nje ya Tanzania .

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamepongeza uamuzi wa mbunge wao kuihama CCM na kujiunga na CCJ.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana walisema CCM sasa kimepoteza dira na kuwakumbatia mafisadi.

Walisema uamuzi huo ni wa busara kwani kwa muda mrefu Mpendazoe alipingwa na viongozi wa CCM wa ngazi zote kutokana na msimamo wake wa kupinga ufisadi.

Walisema licha ya mbunge huyo kujitahidi kuwaletea maendeleo katika jimbo hilo, lakini juhudi zake zimekuwa zikikwamishwa na viongozi wa CCM kwa kushirikiana na viongozi wa serikali hasa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga kwa kumfanyia majungu ili aonekane hafai kwa wanannchi.

“Mpendazoe amejitahidi sana kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jimbo hili ambalo ni wilaya mpya, lakini juhudi zake zote zimekuwa zikikwamishwa na viongozi wa CCM kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali hasa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga na hivyo kumfanyia majungu ili tumuone hafai,� alisema Asha Juma.

Walisema mbunge huyo amekuwa akiandamwa na mambo mbalimbali ambayo hayana msingi hata kuzuliwa kesi ili aweze kupatikana na hatia na hatimaye kufungwa na kupoteza sifa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Pia waliongeza kwa kueleza kuwa uongozi wa CCM Mkoa wa Shinyanga ulikuwa ukisambaza vipeperushi vya kumkashifu mbunge huyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ambapo hufanyika minada kila juma lengo kubwa ni kumchonganisha na wapigakura.

Aidha, walisema CCM ilikuwa imemwandaa mfanyabiashara mmoja maarufu mwenye asili ya Kiasia kuchukua nafasi yake.

Walisema viongozi wa CCM Mkoa wa Shinyanga hawataki wabunge wasomi na wenye msimamo unaosimamia ukweli kutokana na kuzoea vitendo vya ubadhirifu kwa kuwa wengi wao walikuwa viongozi ndani ya Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga(SHIRECU)ambacho kimefilisika kutokana na matumizi mabaya.

Habari hii imeandaliwa na Habel Chidawali, Dodoma, Suzy Butondo, Samwel Mwanga-Shinyanga, Hemed Kivuyo, Arusha.

No comments:

Post a Comment