Thursday, April 1, 2010

MPENDAZOE Januari: CCM ‘Damdam’ Machi: ‘Damdam’ CCJ

BAADA ya Januari mwaka huu kuhojiwa na wanahabari kuhusu uvumi wa kujiunga na Chama Cha Jamii (CCJ) akakana, aliyekuwa Mbunge wa Kishapu kwa tiketi ya CCM, Fred Mpendazoe, ametangaza rasmi kujiunga na chama hicho.

Akihojiwa na gazeti hili mwanzoni mwa mwaka huu, kuhusu CCJ na uhusiano wake na viongozi wa chama hicho, Mpendazoe ambaye amekuwa pamoja na baadhi ya wabunge wakijinadi kupambana na ufisadi nchini, alisema: “Siwezi kuzungumzia mambo ya CCJ kwa sababu mimi ni CCM na huyo Mubhi (Renatus - Katibu Mkuu wa muda) si ndugu yangu na nasikia anatoka mkoa wa Mara … hata angekuwa ndugu yangu kuna tatizo? Mbona Slaa (Wilbrod) yuko Chadema na mkewe CCM na wanaishi pamoja? Kila mtu ni mtu mzima.” Aliongeza kusema yeye bado ni mwana CCM na ni mwakilishi wa watu na wanaomhusisha na CCJ wanaweza kuwa na nia yao mbaya.

Lakini akitangaza Dar es Salaam jana kuhama CCM, mbunge huyo wa zamani alisema: “Nimefuatilia kwa karibu na kusoma Katiba ya CCJ. Nimeishi kwa matumaini kwa muda mrefu, nikitarajia siku mambo yatabadilika ndani ya CCM, mpaka leo sioni dalili yoyote. Nimeona ni heri niheshimu dhamira yangu, kama Mwalimu Julius Nyerere, alivyotuasa kuwa CCM si Helena (mama yake mzazi).

”Nasononeka CCM imegeuka kimbilio la kila mwenye dhamira ya ulanguzi, CCM imepoteza maadili ya uongozi na imekuwa ngome ya mafisadi wanaotafuna utajiri wa nchi yetu.”
Aliongeza: “CCJ ni kama Yoshua aliyewapeleka Kanani. Hakuna ubishi CCM imetutoa Watanzania katika Ukoloni, imefanya kazi kubwa, imefikia kilele chake lakini nasema haiwezi tena kuwapeleka Watanzania kwenye mabadiliko ya karne hii, tunahitaji fikra na mtazamo mpya ambao haina.

CCJ ndiyo itakayotupeleka kwenye mabadiliko ya kweli na ya dhati.” Wabunge wengine wa CCM ambao walikana kuhusishwa na CCJ ni pamoja na John Shibuda (Maswa), Anthony Diallo (Ilemela) na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela). Vigogo wengine waliokana ni Mawaziri Wakuu wa zamani, John Malecela na Joseph Warioba. Naye Mubhi kwa upande wake, alikana kuwa na uhusiano na Mpendazoe, akisisitiza kuwa hata hamfahamu.

Mwenyekiti wa CCJ, Richard Kihabo alisema jana kuwa Mpendazoe amejiunga na chama chake si kwa sababu ya kutafuta cheo, bali kutoa mchango wake katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa. “Ametangaza kujiunga na chama kwa lengo la kutoa mchango wake na si kufuata cheo hapa, mtu yeyote anayetaka kujiunga na chama anaruhusiwa ili mradi asivunje sheria,” alisema. Kwa upande wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, alisema chama chake kimezisikia taarifa hizo kijuujuu, lakini kwa mujibu wa Katiba Ibara 13 (1) (a) mwanachama yeyote akijiunga na chama kingine amejivua uanachama CCM.

Alisema CCM pia inatambua kuwa ni haki ya mwanachama awe kiongozi au la, kuhama chama na kwenda kingine. “Na huyu Mpendazoe ametumia haki yake hiyo, CCM tuna wanachama zaidi ya milioni 4.6 hivyo hatotuathiri kuondoka kwake,” alisema.

Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 71, mbunge anapohama chama anapoteza moja kwa moja sifa ya kuwa mbunge. “Kwa lugha ya kibunge huwa tunaita crossing floor, hapo hupoteza ubunge na sifa zake zote,” alisema.

Alisema taarifa za Mpendazoe kujiunga CCJ wamezipata lakini si rasmi na chama chake cha awali cha CCM ndicho chenye jukumu la kutoa taarifa katika Ofisi za Bunge, kuhusu kujiondoa kwa mbunge huyo. Hata hivyo, Msekwa alipingana na hilo na kutoa mfano wa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Mrema, ambaye akiwa mbunge wa Moshi Vijijini alihama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

“Haikuhitajika kupelekwa taarifa, tamko alilotoa kwenye mkutano wa hadhara lilitosha kabisa kumwondolea sifa ya ubunge, hali ambayo ni sawa na hii ya Mpendazoe ambaye leo (jana) tumemsikia ametangaza mwenyewe tena hadharani kujiondoa CCM, inatosha kabisa kumwondolea sifa ya ubunge.” Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Rajab Kiravu, alisema hata kama mbunge huyo atakuwa amejiondoa na chama kilichompitisha kuridhia na jimbo kuwa wazi, nafasi hiyo haitazibwa mpaka uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, hakuwa tayari kusema lolote badala yake alimpa jukumu hilo Ofisa Habari Mwandamizi wa Bunge, Ernest Zulu, ambaye kama bosi wake, hakuwa tayari kuzungumza zaidi.

“Ninachoweza kusema hapa ni kwamba ofisi ya Bunge inasubiri barua kutoka wale waliowaletea orodha ya Wabunge ambao ni Tume ya Uchaguzi.” Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda aliyetakiwa kuzungumzia haki za mbunge anayehama chama, ikiwamo hatma ya mafao yake, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa alikuwa safarini.

“Nipo huku porini na sikusikii vizuri na nimechelewa utanisamehe.” Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alisema amepokea uamuzi wa Mpendazoe kwa mshtuko mkubwa na ataamini jambo hilo atakapoambiwa na Mpendazoe mwenyewe.

“Mpendazoe amekuwa karibu sana nami na hakuwahi kunielezea azma yake ya kuondoka CCM,” alisema Lembeli. “Kwa hali ya kawaida kuhama chama sasa hivi ni jambo zito, uamuzi wake ni sawa na mtu anayeamua kujinyonga anafikia hatua ya kufanya hivyo baada ya kuona hakuna suluhisho lingine,” alisema.

Naye Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), alisema amesikitishwa na uamuzi huo kwani ni habari mpya na ngumu kwake na hata kuelezea inakuwa ngumu. Selelii alipoulizwa kama na yeye ana nia hiyo alisema, “wapo watakaokwenda huko lakini si mimi … mimi ni mwanachama wa CCM na nitaendelea kubaki CCM hata kama si kiongozi.”

Lucy Owenya (Chadema) alisema, “kama kaamua kuhama Katiba inamruhusu…huyu anajua matatizo yaliyoko ndani ya CCM ndiyo maana kaamua kuondoka,” alisema Owenya.

Elieta Switi (CCM), alisema kuhama ndiyo maana halisi ya demokrasia, kwamba mtu habanwi kuwa katika chama kimoja na kuongeza, “kazi ni kwake huko alikokwenda, lakini nadhani yeye anaona amefanya uamuzi sahihi na ana sababu ya kufanya hivyo”.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kupitia mtandao wa kompyuta alisema ni uamuzi wa kishujaa kwamba anaweza kutoka na kujiunga na kambi ya Upinzani.

“Tunamkaribisha. Nina shaka na 'strategy (mkakati)' ya kutoka kwa kuzungumza na waandishi wa habari pale MAELEZO na si mkutano jimboni mwake maana hatakuwa mbunge tena kwa kipindi kilichobaki. “Inawezekana amenusa kitu kuwa jamaa wanamtosa, maana nimesikia kulikuwa na Kamati Kuu ya CCM,” alisema.

Kuhusu mafao, alisema hukokotolewa kwa mujibu wa muda ambao mbunge ametumikia. Hata mbunge akifariki dunia sehemu ya mafao yake hulipwa kwa familia yake.

Mbunge mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema huenda Mpendazoe amehisi kuwa hatapita katika kura za maoni CCM, kutokana na madai kuwa matajiri wameshammaliza, hivyo atapitia CCJ kuwania ubunge.

Kabla ya kuhama CCM, Mpendazoe amekuwa akikabiliwa na vitimbi mbalimbali jimboni mwake, ikiwa ni pamoja na kusambazwa vipeperushi kwenye mnada wa mifugo na mitaa ya mji mdogo wa Mhunze, wilayani Kishapu, vikimtuhumu kwa kutotimiza ahadi zake.

Baadhi ya vipeperushi vilisomeka: 'Mpendazoe ulitudanganya kuwa tukikuchagua ubunge utateuliwa kuwa Waziri, mbona hata unaibu Waziri hukuteuliwa!' 'Mpendazoe wananchi wa Kishapu hatukutaki uwe mbunge wetu, ukigombea tena 2010 tutakuaibisha!

Vingine: ‘Mpendazoe umeivuruga halmashauri ya wilaya ya Kishapu sasa unataka kukivuruga Chama Cha Mapinduzi, chunga kauli zako’. Hata hivyo akivizungumzia, alisema ni sehemu ya utekelezaji wa mafisadi kuwaondoa bungeni baadhi ya wabunge wanaopinga vitendo hivyo.

Alidai mafisadi wametenga Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuwang’oa na kuwamaliza wasisikike kabisa. Hata hivyo, alisema hatishiki na vipeperushi hivyo, kwa kuwa wanaovisambaza wamefilisika kisiasa na ni woga kwa kuwa hawajitokezi hadharani na kwenye vikao halali kutoa madukuduku yao.

Alijinasibu kuwafanyia mambo mengi wapiga kura wake na akawa na imani kuwa wananchi hao watavipuuza na kuendelea kumuunga mkono. Habari zaidi zilidai kuwa mbunge huyo alisababisha kuibuka makundi mawili jimboni mwake; linalomuunga mkono na linalompinga, huku ikidaiwa kuwa alishitakiwa kwa Spika Samuel Sitta na aliyekuwa msaidizi wake katika uchaguzi wa mwaka 2005 kwa madai ya kumdhulumu.

Katika kukanusha tuhuma hizo, Mpendazoe alikiri kufahamiana na msaidizi wake huyo na kusema alishamsaidia mambo mengi, lakini hakumlipa fedha zake kutokana na kumchafua na kutoa siri zake sehemu mbalimbali.

“Huyo bwana namjua ni ndugu yangu, ni kweli tulikuwa na makubaliano fulani ambayo mimi sijayatekeleza, lakini ameniudhi sana baada ya kuzunguka sehemu mbalimbali na kuanza kutoa siri zangu,” alikaririwa na gazeti moja nchini.

“Kote alikokwenda wamempuuza, amefika hadi kwa Spika, NEC, PCCB hadi Polisi ili kunichafua, lakini wamempuuza, sasa anatumia vitisho ili nimlipe, kwa nini?” Mpendazoe pia alituhumiwa kumtisha kwa bastola Abdulkadir Mohamedi, ambaye pia ni kada wa CCM Kishapu.

Ilidaiwa kuwa Mbunge huyo wa zamani alimshambulia Mohamedi kwa makofi, kumchania nguo na kumtishia bastola, lakini alikanusha akidai ni uongo dhidi yake wenye lengo la kumchafua kisiasa.

No comments:

Post a Comment