Thursday, April 1, 2010




ICS yatumia milioni 226 Meatu
Shirika lisilo la kiserikali la International Child Support (ICS) limetumia kiasi cha sh 226, 386, 500 wilayani Meatu mkoani Shinyanga, kwa kipindi cha mwaka 2004/ 2005 kutekeleza mpango wa kusaidia mtoto shuleni.

Hayo yalisemwa na Meneja Miradi wa shirika hilo nchini, Bi. Doroth Ndege, aliposoma taarifa ya utekelezaji wa mpango huo kwa Afisa wa Tarafa ya Kisesa, Bw. Fabian Mgina.

Alisema hayo wakati akifungua makambi ya afya kwa shule za msingi wilayani hapa katika Kijiji cha Mwakoluba.

Bi. Ndege alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja, shirika lake limetekeleza miradi mitatu ambayo ni kusaidia mtoto shuleni, ufadhili wa watoto yatima na utunzaji wa nafaka katika kijiji cha Mwabusalu.

Alisema malengo ya mpango wa kumsaidia mtoto shuleni, ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na huduma za kiafya katika shule za msingi, kuimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali na kusogeza huduma za maji kwa watoto shuleni.

Bi. Ndege alisema shirika lake pia limeweza kuhamasisha jamii katika ushiriki wa miradi ya maendeleo kupitia serikali za vijiji na kamati za shule, kwa kujenga vyoo na kutengeneza samani katika shule zote zilizoko kwenye mradi huo.

Alisema hadi sasa madawati 1,600, viti 224, meza 224 na kabati 80, vimetolewa na shirika hilo katika shule 16 za tarafa za Kimali, Kisesa na Nyalanja.

Kutoka gazeti la Nipashe

No comments:

Post a Comment