BIBI Milembe Ndugulile (81), ambaye ni mkazi wa mkoa wa Shinyanga vijijini, ametoa mchango wa sh 200 ukiwa ni mchango wake kwa Rais Jakaya Kikwete ili kumwezesha kununua fomu ya kuwania tena urais endapo ataamua kufanya hivyo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Idara ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, imeeleza kuwa bibi huyo, ametoa mchango wake huo wa sarafu moja ya sh 200 katika mchango wa jumla wa wananchi wa Shinyanga wa kumwunga mkono Rais Kikwete katika kinyang’anyiro cha kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
Mchango huo ulikuwa miongoni mwa sh 1, 482,200, ambazo alikabidhiwa Rais Kikwete na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, katika halfa fupi iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Katika risala iliyosomwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Mkoa wa Shinyanga, Stepehen Masele, kabla ya Ngeja kukabidhi fedha hizo, ilielezwa kuwa fedha hizo zilitokana na michango ya hiari ya papo kwa hapo ya wananchi wa Shinyanga, wakati wa tafrija ya kuwasimika makamanda wapya wa UVCCM wa mkoa huo, iliyofanyika Machi 3, mwaka huu, mjini Shinyanga.
Mwenyekiti huyo wa mkoa alimweleza Rais Kikwete kuwa Bibi Milembe Ndugulile alikuwa amesisitiza kuwa fedha hizo (sarafu moja ya sh 200) zifikishwe kwa Rais Kikwete, kama mchango wake binafsi kuonyesha furaha yake kwa uongozi wake katika miaka minne iliyopita.
“Bibi Ndugulile ameniagiza nikuambie kuwa sh 200 ndiyo uwezo wake na ni fedha ndogo, lakini ni ishara ya kuonyesha dhamira yake kuwa ataendelea kuunga mkono uongozi wako kutokana na mengi ambayo umeifanyia nchi hii katika miaka minne iliyopita katika kulinda utaifa, umoja, mshikamano, amani na utulivu,” alieleza Ngeja.
Akitoa shukurani zake, Rais Kikwete, alisema ameupokea kwa dhati mchango huo wa Bibi Ndugulile na kwamba ni muhimu sana kwake.
“Mchango huu ni muhimu sana kwangu, ni mchango unaoonyesha upendo wa bibi huyo kwangu na utanisaidia kuifanya hiyo kazi, baada ya uamuzi kuwa umechukuliwa kuhusu suala hili.”
No comments:
Post a Comment